Saturday, August 15, 2009

TAARIFA YA HABARI AGOSTI 15, 2009

HABARI ZA KITAIFA

Zanzibar,
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Kiongozi, katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Bwana Hamza Hassan Juma, ameipuuza taarifa ya Jumuiya ya Ulaya kwa madai kuwa imetolewa bila ya kufanyiwa utafiti wa kutosha.

Waziri Hamza, amesema kimsingi hakuna mwananchi mwenye sifa aliyenyimwa kuandikishwa kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kisiwani Pemba kwa lengo la kisiasa.

Waziri Hamza, ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kusimama kwa uandikishaji wa daftari hilo kutokana na vurugu zilizotokea vituoni ikiwa ni siku moja baada ya jumuiya hiyo kusema kuwa kuna kasoro zimejitokeza kwenye zoezi hilo.

Kutokana na kasoro hizo, Jumuiya ya Ulaya jana imezitaka Serikali za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mapinduzi ya Zanzibar kurekebisha hali hiyo ili kuhakikisha kila Mzanzibar anapata haki yake ya kujiandikisha kwenye daftari hilo.

Hata hivyo, Waziri Hamza, amesema chanzo cha matatizo yaliyojitokeza katika zoezi hilo ni kutowajibika ipasavyo kwa viongozi wa majimbo kwa madai kuwa wabunge na wawakilishi wameshindwa kutoa elimu mapema kuhusu taratibu zinazopaswa kufuatwa na wananchi kabla ya kupewa kitambulisho cha Uzanzibari Ukaazi.

Amesema, wananchi wengi wanaolalamika kuwa hawana vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi hawana vyeti vya kuzaliwa kama inavyotakiwa hivyo amewataka wananchi wasio na sifa kwenda mahakamani kula kiapo na kufuatilia vyeti vya kuzaliwa.

Zoezi hilo sasa linatarajiwa kufanyika Agosti 17.

Singida,
WANAFUNZI
wa kidato cha Nne katika shule ya Sekondari ya Nduguti iliyopo wilayani Iramba mkoani Singida wamemjeruhi mkuu wa shule hiyo, Bwana Evan Mombo, baada ya kumshambulia kwa bakora na mawe wakishinikiza kupatiwa matokeo ya mtihani wa majaribio.

Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Singida, Bibi Celina Kaluba, amesema tukio hilo limetokea jana baada ya wanafunzi hao kudai matokeo hayo kwa muda mrefu bila ya mafanikio.

Kamanda Kaluba, amesema mwalimu huyo amejeruhiwa vibaya kwa kucharazwa na fimbo sehemu mbalimbali mwilini kabla ya kupigwa kwa mawe na kujeruhiwa kichwani.

Amesema, wanafunzi hao wamefikia hatua ya kufanya fujo hizo baada ya kuchoshwa na ahadi zisizotekelezwa kutoka kwa mwalimu huyo kila wanapotaka kupatiwa majibu hayo.

Kamanda Kaluba, amesema hali ya mwalimu huyo inaendelea vizuri baada ya kupatiwa matibabu kwenye zahanati ya kijiji hicho.

Dar es Salaam,
KESI
ya wizi wa zaidi ya shilingi bilioni moja kupitia Akaunti ya Madeni ya Nje, EPA katika Benki Kuu ya Tanzania, BoT, inayowakabili wamiliki wa Kampuni ya Changanyikeni Residential Complex, inatarajiwa kusikilizwa mfululizo kuanzia Septemba 28 hadi Oktoba 12 mwaka huu.

Upande wa mashtaka unatarajia kuwasilisha mashahidi 23 ambao wanatarajiwa kutoa ushahidi dhidi ya washtakiwa, Bahati Mahenge, Manase Mwakale, Davis Kamungu, Godfrey Mosha na Eda Mwakale.

Mahakimu wanaotarajiwa kuiskiliza kesi hiyo ni Sekela Moshi, Sam Rumanyika na Lameck Mlacha, ambao watafanya kazi hiyo kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam.

Taarifa hiyo imetolewa leo na Hakimu Mkazi wa mahakama ya Kisutu, Bibi Eva Nkya, wakati kesi hiyo ilipotajwa kwa lengo la kupangiwa tarehe ya kuendelea kusikilizwa.

Dar es Salaam,
WIZARA
ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, imekemea vikali kitendo cha kikatili alichofanyiwa mtoto, Alex Mwingizim mwenye umri wa miaka 14, ambaye ameunguzwa kwa maji ya moto na mama yake, Bibi Maria Madenge.

Serikali imetoa kauli hiyo kufuatia taarifa zilizotolewa jana na gazeti la Majira ambazo zimeambatana na picha ya mtoto huyo ikieleza jinsi alivyofanyiwa ukatili huo.

Katika taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari na kusainiwa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Bibi Mariam Mwaffisi, imebainisha kuwa matukio ya aina hiyo ndiyo yanayorudisha nyuma juhudi za Serikali na wananchi katika kupiga vita ukiukaji wa haki za watoto.

Wizara imesema watoto wanapaswa kulindwa dhidi ya vitendo vya ukatili kama ilivyotamkwa katika mikataba ya kimataifa ya haki na ustawi wa mtoto ambazo Tanzania imeziridhia.

Dar es Salaam,
WATU
wawili wamekufa katika matukio mawili tofauti yaliyotokea juzi jijini Dar es Salaam kutokana na ajali za barabarani.

Akitoa taarifa hizo jana, Kamanda wa Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna Seleiman Kova, amesema tukio la kwanza limetokea eneo la Bagamoyo New Fao wilayani Kinondoni baada ya mkazi wa Tandale, Masima Yohana, kugongwa na gari na kufa papo hapo.

Kamanda Kova, amesema gari hiyo iliyokuwa ikitokea Moroko kuelekea Bagamoyo na dereva wake ametoroka mara baada ya tukio hilo.

Amesema, tukio hilo limetokea juzi saa tatu usiku na maiti ya mtu huyo imehifadhiwa katika hospitari ya Mwananyamala huku juhudi za kumtafuta dereva huyo zinaendelea.

Katika tukio la pili lililotokea eneo la Kimara Kisauni wilaya ya Kinondoni, mtu mmoja mtembea kwa miguu ambaye jina lake halijafahamika anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 35 amekufa mara baada ya kugongwa na pikipiki aina ya bajaji.

Kamanda Kova, amesema tukio hilo limetokea juzi saa moja usiku ambapo pikipiki hiyo yenye namba T 715 ASK ilikuwa ikiendeshwa na mfanyabiashara Bwana Jack Richard, mkazi wa Mwananyamala akitokea Kimara Baruti kuelekea Mwananyamala Mwisho.

Mwili wa marehemu huyo umehifadhiwa katika hospitari ya Mwananyamala na dereva huyo anashikiliwa kwa uchunguzi zaidi.

HABARI ZA KIMATAIFA

Lusaka,
KESI
ya ufisadi inayomkabili Rais wa zamani wa Zambia, Bwana Frederick Chiluba, jana imeahirishwa hadi wiki ijayo ukiwa ni muda wa miaka sita tangu ilipoanza kusikilizwa.

Bwana Chiluba, anadaiwa kutumia vibaya takriban dola 500,000 za Marekani ambazo ni mali ya umma wakati akiwa Rais wa Zambia kuanzia mwaka 1991 hadi mwaka 2001.

Taarifa kutoka mjini Lusaka zinasema kuwa Hakimu anayeiendesha kesi hiyo, Bwana Jones Chinyama, ameiahirisha kwa sababu hakuwa tayari kutoa uamuzi na hakutokea mahakamani hapo.

Bwana Chiluba, alikuwa na watuhumiwa wengine anaoshtakiwa nao katika kesi hiyo pamoja na mke, Bibi Regina Chiluba, ambaye hivi karibuni ameshinda rufaa ya kifungo cha miaka mitatu na nusu jela adhabu aliyohukumiwa Machi mwaka huu.

Taipei,
ZAIDI
ya watu 390 wanasadikika kuwa wamezikwa wakiwa hai kwenye vijiji vilivyoathirika na maporomoko ya udongo Kusini mwa Taiwan kutokana na kimbunga kilichotokea mwishoni mwa wiki iliyopita.

Taarifa ya Serikali ya Taiwan, imesema watu hao wamefukiwa baada ya kukosa msaada wa haraka wa kuwaokoa kutoka kwenye maeneo hayo na hadi sasa bado kuwa watu kadhaa ambao wamekwama katika maeneo yasiweza kufikiwa kwa urahisi.

Serikali ya Taiwan imetoa taarifa hiyo jana ikiwa ni siku moja baada ya kuomba msaada wa Jumuiya ya Kimataifa ili kufanikisha kuwaokoa zaidi ya watu 200 waliokwama kwenye maeneo yaliyokumbwa na kimbunga hicho.

Hii ni mara ya kwanza kwa Serikali ya nchi hiyo kutoa idadi ya watu wanahofiwa kupoteza maisha yao kutokana na kimbunga hicho huku kukiwa bado kuna watu wamekwama kwenye maeneo mbalimbali kutokana na maporomoko ya udongo na mafuriko.

Kimbunga hicho kimesababisha mafuriko ambayo hayajawahi kutokea katika kipindi cha miaka 50 iliyopita katika historia ya nchi hiyo.

Tehran,
MMOJA
kati ya waliokuwa wagombea wa upinzani katika uchaguzi mkuu wa Rais uliofanyika Juni 12 nchini Iran, Bwana Mehdi Karroubi, amedai baadhi ya waandamanaji waliokamatwa kwenye ghasia za kupinga matokeo ya uchaguzi huo wamekufa kutokana na mateso waliyoyapata wakiwa gerezani.

Bwaana Karroubi, ametoa madai hayo jana ikiwa ni siku chache baada ya kusema kudai kuwa idadi kubwa ya mahabusu wanawake na wanaume walibakwa wakati wakiwa rumande.

Hata hivyo, Maofisa wa Serikali ya Iran wamekanusha taarifa hizo licha ya kukiri kuwepo kwa vitendo vya udhalilishaji.

Kutokana na madai hayo, Bwana Karroubi, ametoa wito wa kuundwa kwa tume huru itakayochunguza suala hilo ili kupata ukweli na kuwezesha kuchukuliwa kwa hatua za kisheria dhidi ya wahusika.