Friday, February 6, 2009

Mugabe kusaini mabadiliko ya katiba

HARARE,
RAIS
Robert Mugabe wa Zimbabwe, anatarajiwa kusaini mabadiliko ya sheria kwenye katiba ya nchi hiyo yatakayomwezesha Kiongozi wa Upinzani kutoka chama cha Movement for Democratic Change, MDC, Bwana Morgan Tsvangirai, kuwa Waziri Mkuu wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Serikali hiyo inaundwa kufuatia kusainiwa kwa mkataba wa kugawana madaraka baina ya chama tawala Zanu-PF na kambi ya upinzani Septemba 15 mwaka jana ikiwa ni hatua ya kumaliza mgogoro wa kisiasa nchini humo.

Baada ya Rais Mugabe kusaini mabadiliko hayo, Bwana Tsvangirai, anatarajiwa kuapishwa rasmi kuwa Waziri Mkuu wa Zimbabwe Jumatano, Februari 11 mjini Harare.

Mabadiliko hayo yamepitishwa hivi karibuni na bunge la Zimbabwe na kutoa nafasi kwa viongozi hao kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Hata hivyo, baadhi ya nchi hisani zikiwemo Marekani na Uingereza pamoja na Umoja wa Ulaya zimeweka wazi misimamo yao kuwa hazitaondoa vikwazo vyao kwa Zimbabwe hadi hapo Serikali hiyo itakapotimiza lengo la kuundwa kwake.

No comments:

Post a Comment