Friday, February 6, 2009

Rais Somalia aomba suluhu na al-Shabaab

ADDIS ABABA,
RAIS
mpya wa Serikali ya mpito ya Somalia, Sheikh Sharif Sheikh Ahmed, ameonesha nia ya kufanya mazungumzo na kundi la al-Shabaab linaloshikilia maeneo mengi muhimu ya nchi hiyo na kuisababisha Serikali yake kushindwa kufanyakazi nchini humo.

Viongozi wa Serikali hiyo hivi sasa wanaishi kwenye nchi za Kenya na Djibouti baada ya kundi hilo kuuteka mji wa Baidoa uliokuwa ukitumiwa na Serikali hiyo kama makao yake makuu.

Sheikh Sharif, amesema njia pekee ya kuleta umoja na mshikano nchini humo na hatimaye kurejesha amani ya Somalia ni kwa Serikali yake kufanya mazungumzo na kundi la al-Shabaab.

Amesema, Somalia kwa sasa inakabiliwa wa ukosefu wa umoja miongoni mwa raia wake huku kila mmoja akidhani kuwa ana haki ya kufanya mambo nchini humo bila ya kuwashirikisha wengine jambo ambalo amesema sasa linapaswa kuondolewa na kujenga Somalia moja.

Sheikh Sharif, alikuwa ni miongoni mwa viongozi wa Umoja wa Mahakama za Kiislam ulioshika madaraka kwa takriban miezi sita kabla ya utawala wao kuondolewa madarakani na majeshi ya Ethiopia na amechaguliwa hivi karibuni na bunge la nchi hiyo kuchukua nafasi ya Rais Abdillah Yusuf Ahmed, aliyejiuzulu Disemba mwaka jana.

No comments:

Post a Comment